BUNGE – HOTUBA YA WAZIRI WA ARDHI – MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI 2012-2013
HOTUBA YA WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, MHESHIMIWA
PROF. ANNA KAJUMULO TIBAIJUKA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA
MAKAZI KWA MWAKA WA FEDHA
2012/2013
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika,naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Bunge lako likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika mwaka 2011/12 na malengo ya Wizara katika bajeti ya mwaka 2012/13. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2012/13.
2. Mheshimiwa Spika,awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Waheshimiwa Wabunge kuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki mkutano huu wa nane wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu kuwa azipokee na kuzilaza pema roho za Waheshimwa Wabunge waliotangulia mbele ya haki tokea mkutano wa Bajeti wa mwaka 2011/12 ulipofanyika.
3. Mheshimiwa Spika, pili, naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais; na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu na Mbunge wa Mpanda Mashariki, kwa uongozi wao mahiri. Nawashukuru kwa ushauri, maelekezo na ushirikiano wanaonipa, ulioniwezesha kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa ya kuongoza sekta hii muhimu katika maendeleo ya nyanja zote za maisha katika Taifa letu. Nawapongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; pamoja na Makamu wake wawili Mhe. Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; na Mhe. Balozi Ali Idd Seif, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar. Kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyoionesha kwangu kwa kuamua niendelee kuongoza Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya mapema mwezi Mei 2012. Napenda kumhakikishia kuwa nitaendelea kujenga timu yenye nguvu ili kwa pamoja tujenge sekta ya ardhi yenye tija kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu.
4. Mheshimiwa Spika, nakupongeza kwa umahiri na umakini ambao umeonesha katika kuongoza shughuli za Bunge. Hongera sana, na Mwenyezi Mungu aendelee kukuongoza na kukupa hekima zaidi. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Mbunge wa Kongwa na Naibu Spika wa Bunge letu kwa kazi nzuri katika kuendesha shughuli za Bunge. Pia, nawapongeza Waheshimiwa Wenyeviti Jenista Joakim Mhagama (Mbunge wa Peramiho), Sylivester Massele Mabumba (Mbunge wa Dole) na Mussa Zungu Azzan (Mbunge wa Ilala), kwa kuongoza vyema shughuli za Bunge tangu wachaguliwe kushika nyadhifa za uenyekiti.
5. Mheshimiwa Spika,naomba nichukue fursa hii kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais katika Baraza la Mawaziri kufuatia mabadiliko aliyoyafanya mwezi Mei 2012:Mhe. Dkt. William Augustao Mgimwa (Mb), kuwa Waziri wa Fedha; Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (Mb), kuwa Waziri wa Nishati na Madini; Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb), kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb), kuwa Waziri wa Uchukuzi; Mhe. Dkt. Fenella Ephraim Mukangara (Mb), kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb), kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii; Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb), kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko. Pia, napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mawaziri katika Wizara mbalimbali: Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb), Wizara ya Fedha; Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb), Wizara ya Fedha; Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii; Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb), Wizara ya Nishati na Madini; Mhe. January Yusuf Makamba (Mb), Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia; Mhe. Dkt. Charles John Tizeba (Mb), Wizara ya Uchukuzi; Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb), Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Mhe. Angela Jasmine Kairuki (Mb), Wizara ya Katiba na Sheria; Mhe. Stephen Julius Maselle (Mb), Wizara ya Nishati na Madini; na Mhe. Mhandisi Dkt. Binilith Satano Mahenge (Mb), Wizara ya Maji. Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochaguliwa na walioteuliwa katika kipindi cha mwaka uliopita kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na Bunge la Afrika. Ni matumaini yangu kuwa watatuwakilisha vyema kwa maslahi na manufaa ya Taifa letu.
6. Mheshimiwa Spika,napenda nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Muleba Kusinikwa kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu yangu nikiwa Mbunge wao. Pamoja na kuwa na kazi nyingi za kitaifa, wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini wamekuwa wakinipa ushirikiano mzuri na kujitahidi kukutana nami ninapopata nafasi kufika jimboni kwa kuhudhuria vikao na mikutano katika tarafa zao au kupokea wageni na wataalaam waelekezi ninaowatuma kufika kusukuma maendeleo yetu. Ninawashukuru sana kwa uelewa na ushirikiano, na uongozi madhubuti wa madiwani na wenyeviti wa vijiji kuunda Mifuko ya Maendeleo ya Kata ambayo italeta mapinduzi katika kupunguza umaskini na kutuletea maendeleo endelevu. Ninawapongeza Madiwani ambao tayari wamesajili taasisi ya mifuko hiyo katika kata za Mubunda, Kyebitembe, Rulanda, Muleba, Bureza, Magata Karutanga, Kimwani, Mazinga, Nyakabango, Nshamba, Kishanda, Buganguzi, Burungura, Buhangaza, Kashasha, Ijumbi, Biirabo na Muleba Mjini. Ninawahimiza wale ambao bado hawajakamilisha zoezi hili wakazane tusonge mbele kwa pamoja. Aidha, natuma salamu kwa vijana wanaoshiriki katika mashindano ya kandanda ya Kombe la Anna Tibaijuka. Ninawapongeza wale ambao wameshinda mashindano ya kata na ninaamini mwisho wa mwaka tutakapocheza fainali washindi wataweza kutoa vijana wa Muleba kujiunga na Taifa Stars. Nimefurahi kusikia kwamba na wasichana hawakubaki nyuma wameitikia wito wangu na kushiriki michezo ya riadha inayotangulia mashindano ya mpira. Vijana michezo ni maendeleo. Kwa wenye vipaji, Muleba tusikubali vijana wetu kubaki nyuma kwa kuwa tu tuko mbali na majiji makubwa nchini hususan Dar es Salaam. Kwa kupitia ligi yetu, wenye uwezo wataibuka na kung’ara na kusonga mbele. Aidha, ninawashukuru ndugu, jamaa na marafiki walionisaidia na kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu ya Uwaziri na Ubunge. Nawashukuru wananchi na kuwahakikishia popote pale mlipo, iwe Tarafa ya Nshamba, Kimwani au Muleba yenyewe, kwamba tutayalinda mafanikio tuliyoyafikia na kuongeza kasi zaidi ili kufikia malengo ya kulinda amani, utulivu na kufikia maisha bora. Namuomba Mwenyezi Mungu amwezeshe kila mwananchi kulitambua hili na kuchangia katika nafasi yake kwa kadri ya uwezo wake kufikia maisha bora. Mwisho ninatuma salamu kwa mama yangu mzazi Ma Aulelia Kajumulo hapo Muleba. Sala zake za kila siku anapokuwa na nguvu zinasikika maana huku mie ni mzima wa afya.
7. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru kwa dhati viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM), viongozi na watendaji wa Serikali kwa kuniwezesha kutekeleza majukumu ya Wizara yangu. Kwa namna ya kipekee natoa shukurani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa James Daudi Lembeli (Mbunge wa Kahama), kwa ushirikiano mkubwa na ushauri wao ambao umeiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Natoa shukurani za pekee kwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Goodluck Joseph Ole-Medeye (Mbunge wa Arumeru Magharibi) kwa ushirikiano na umoja tuliojenga kutekeleza majukumu yetu na pia nampongeza kwa Mhe. Rais kuamua aendelee na wadhifa wake huo. Nawashukuru pia Katibu Mkuu Bw. Patrick Rutabanzibwa; Naibu Katibu Mkuu, Bibi Maria Bilia; watendaji katika Idara, Vitengo, Shirika na Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa ushauri na mshikamano wao katika kupanga na kutekeleza mipango ili kufikia malengo tuliyojiwekea. Watanzania wengi wanatambua changamoto kubwa zinazoikabili sekta yetu lakini hakuna kinachoshinda umoja, maana ni nguvu ya pekee.
Ili kusoma hotuba kamili bonyeza viunganishi(links) hapa chini
Posted by Noel Mubeya
on Jul 16 2012. Filed under Parliament.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0.
Both comments and pings are currently closed.