Prof  Anna Kajumulo Tibaijuka

MADAWA YA KULEVYA, VIROBA NA SIGARA – HATARI TUPU KWA VIJANA WASIOWEZA KUJIZUIA – (Sehemu ya Kwanza).

Na  Profesa Anna Tibaijuka
Vita dhidi ya madawa ya kulevya hivi sasa ndilo jambo linalotawala shughuli za taifa letu. Jambo hili ni mojawapo ya matunda na mafanikio ya Serikalli ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli. Yeye na majemadari wake katika vita hii wanastahili pongezi na ushauri na si kejeli wanapokosea.
Nitatofautina na wengi nikianza basi kwa kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Paul Makonda, kwa kuthubutu kuendesha vita hii ingawaje nilikuwa mtu wa kwanza kusema kwamba ingelikuwa bora zaidi kutafuta ushahidi kabla ya kutangaza majina ya watuhumiwa. Jambo ni kubwa. Nimefarijika kuona kasoro hii sasa imezingatiwa, kwani majina 97 bado hayajawekwa hadharani bali yanafanyiwa kazi na mamlaka husika na polisi.
Hakuna shaka wakikuta kuna ushahidi wakutosha tutajua tu watuhumiwa ni akina nani na wenye hatia watajulikana mahakamani. Hii ndiyo dunia ya wastaarabu na utawala bora na wa haki ilivyo.

Kamishna Mkuu wa kitengo cha madawa ameteuliwa na Kamanda wa Kikosi Maalum wanaonekana hawatalaza kazi. Ni timu ya mauaji! Haionekani kama itashindwa kazi. Tuwaombee Baraka za Mwenyezi Mungu maana jukumu walilopewa ni gumu sana.
Kama sikubaliani na utangazaji wa majina kwa watuhumiwa, tena kwa mbwembwe, kwa nini ninampongeza basi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam? Nina sababu tatu za msingi. Kwanza ninampongeza kwa utayari wake kulitumikia taifa hili. Pili ninampongeza kwa kuanza kwa mwendo kasi. Pamoja na ukakasi wa kutangaza majina, imesaidia kuamsha taifa lililokuwa limesinzia kana kwamba tatizo halikuwepo. Tatu ninampongeza kwa kukubali lawama na kujaribu kujitetea.

Mwalimu Nyerere, Baba wa Taifa wakati anangatuka alisema kwamab kama kiongozi amefanya makossa mengi, na katika hilo anaomba wananchi wamsamehe. Lakini alisema kama kiongozi hajafanya madhambi kwa hiyo hana sababu ya kuhofu kuondoka madarakani na kung’atuka. Ili nisiwachoshe kwenye mtandao huu, nitaleta Makala yangu katika awamu tatu.

Leo nitashughulikia tu jambo la kwanza. Kumpongeza Makonda kwa utayari wake kulitumikia taifa hili.
Taka usitake, amejitoa mhanga. Kukubali kufanya kazi ngumu kuliko zote duniani. Kupambana na madawa ya kulevya. Historia imesheheni mifano ya athari zinazoweza kukukumba katika vita hii hata kupoteza nafasi ya kazi yako na hata maisha yako. Kama sio wewe hata familia au jamaa zako wanaweza kuumizwa au kuhujumiwa na mitandao hiyo ya watu wasio na dhamira. Kwa kuwa biashara hii haramu ina faida kubwa, mitandao yake nayo haina simile. Iko tayari kupambana na kumshughulikia yeyote atakayejaribu kuwazuia kufanikisha biashara hiyo.

Ni Dhahiri vita hii jemadari wake hawezi kuwa mkuu wa mkoa hususan Mhe Makonda. Inahitaji nguvu ya Mkuu wa Nchi mwenyewe kuweza kufika mahala popote Lazima uwe na utashi wa kisiasa kufanikiwa (political will). Hii si Tanzania tu bali ni kote duniani. Na Mkuu wa Nchi yeyote anayetaka kupambana na balaa hili naye sharti awe jasiri wa majasiri. Kama anavyosema Rais Magufuli lazima awe mkweli na mpenzi wa Mungu. Ndiyo maana nadhani tatizo hili sasa limepata muarobaini katika Dk. John Pombe Magufuli. Siyo kazi rahisi hii. Nilipokuwa Umoja wa Mataifa nilishuhudia ugumu wake. Shirika la umoja wa Mataifa la Kupambana na Madawa ya Kulevya (UNODC) lenye makao yake makuu Vienna nchini Austria lilikuwa linashirikiana nami hapo UNHABITAT katika Makazi, mitaa duni mijini kuwanusuru vijana. Pamoja na jitihada kubwa, hatukufanikiwa sana.

Nitoe mfano wa kihistoria. Katika miaka ya nyuma, karne ya 18, Waingereza ndio walikuwa wanaongoza katika biashara ya bangi (opium). Wafanyabiashara kutoka Uingereza walileta bangi katika nchi ya Uchina kutoka makoloni yao ya India na Uturuki. Wakawarubuni na kuwafundisha wananchi kutumia bangi kwa kiburudisho na starehe. Kabla ya hapo ilitumika tu kama dawa. Waingereza wakanogewa na faida kubwa itokanayo huku wakiungwa mkono na Serikali yao. Mfalme wa Uchina (Ching dynasty) akaona taifa lake linaangamia kwa kutumia bangi na madawa ya kulevya!. Akapiga marufuku biashara hiyo haramu. Matokeo? Waingereza wakaanzisha vita dhidi yake, wakamshinda na kumlazimisha kuwapa kisiwa cha Hongkong wakitawale na kufungua bandari nyingi ambazo sasa ikawa ruksa kuingiza madawa ya kulevya. China ikapoteza dira.
Hatimaye Mfalme akadhoofishwa na mwisho utawala wa kifalme wa China ukaondolewa madarakani na wanamageuzi. Vita hizi zinajulikana kama “Opium Wars” “Vita vya Bangi”. Vita ya kwanza ilikuwa mwaka 1839-1842. Vita ya pili ni mwaka 1856 – 1860. Kama alivyosema mwanaharakati mweusi wa Marekani, Malcom X. “Serikali inatangaza vita dhidi ya mtu anayekataa kutumia madawa ya kulevya”. Ama kweli madhambi yamefanyika duniani.
Kwa hiyo kiongozi yeyote anayetangaza vita dhidi ya madawa ya kulevya anahatarisha utawala wake. Pamoja na madai kwamba dunia ya wakubwa itazisaidia nchi maskini kupambana na madawa ya kulevya jambo hili lazima tuwe na tahadhari nalo. China ilihangaika na madawa mpaka mwaka 1949 Mwenyekiti Mao Tse-Tung wa Chama cha Kikomunisti alipochukua madaraka na kuondoa ufisadi katika taifa la China. Ndipo akafanikiwa. Penye ufisadi huwezi kuondoa madawa ya kulevya!. Ndio ukweli mweupe. Unakuwa na mitandao ya uovu ikilinda madawa kuanzia Ikulu, hadi Usalama wa Taifa, hadi Polisi, hadi kwenye mashamba ya kulima bangi, viwanda vya kuikamua na mitaa ya kuuza!. Kwa kuwa Rais wetu ameanza na kupiga vita mitandao ya kifisadi, tuendelee kumuombea. Inshallah atafanikiwa!
Katika dunia ya sasa, mitandao ya kifisadi katika vyombo vya utawala ndiyo inadumisha biashara ya madawa ya kulevya. Mfano mwingine. Biashara ya sasa inamilikiwa na watu wakubwa Ulaya na Marekani. Soko kubwa lipo kule. Kwa nini Serikali za kule zimeshindwa kuiongoza biashara hiyo haramu? Mitandao ya mafisadi inailinda. Mfano. Sio siri kwamba katika miaka ya 60 Shirika la Usalama na Ujasusi la Marekani (CIA) liliaminika kujiingiza katika biashara hiyo haramu, likisaidia kusambaza madawa ya kulevya katika mitaa ya watu maskini, wengi weusi, ili kuwaangamiza na lenyewe kujipatia fedha kuendesha vita dhidi ya tawala nyingine katika nchi za nje hususan Laos, Nicaragua, na nchi nyingine walipokuwa hawapendi watawala wake.

Kwa kifupi agenda za kutaka taifa letu liangamie katika bangi na madawa ya kulevya zipo. Sio kila mtu anatutakia mema.
Vita ya madawa ya kulevya inataka uelewa mkubwa wa maswala haya na mazingira yake. Inataka umoja na mshikamano wa kitaifa. Inataka uvumilivu na si kunyosheana vidole. Kazi kubwa mbele yetu ni kuwanusuru vijana wetu wasiingie katika balaa hili. Uwezo wetu kuwasaidia ni mdogo sana. Kinga ni bora kuliko tiba. Ndiyo maana nasema Makonda ni jasiri na wote waliopewa jukumu hili wana kazi ngumu. Tuwaunge mkono.
Katika sehemu ya pili ya Makala hii nitazungumzia mafanikio ya mwendo kasi wa Makonda. Tayari katuzindua usingizini kama Taifa. Ni “Shock therapy”. Kama ni kosa sio dhambi. Tumsamehe na kumuunga mkono. Tupigane kwa pamoja. Wachina nao walifanikiwa hivyo hivyo. Kwa mwendo kasi hadharan

Posted by on Feb 22 2017. Filed under Prof Tibaijuka's Daily Photo News. You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Both comments and pings are currently closed.

Comments are closed

Photo Gallery

Log in | This website is Designed & Maintained by Noel Mubeya